SADAKA IGUSAYO

Sehemu  tatu za sadaka igusayo moyo wa Mungu

  • Kutoa miili yetu kama sadaka na dhabihu takatifu iliyo hai.

  • Kutoa muda wako kama dhabihu takatifu iliyo hai ili ikamfanyie yeye manukato.

  • Kutoa mali na fedha zako kwa ajili ya kumtumikia BWANA.

Katika maeneo yote haya Mungu alifanya ili mwanadamu afurahie uzuri na uaminifu wa Muumba wake, na anafurahi sana kuona mwanadamu anashiriki pamoja naye na kumshirikisha katika kila jambo ampalo.

  1. Kutoa miili kama dhabihu iliyo hai ya kumpendeza Mungu 

Maandiko matakatifu katika kitabu cha Warumi 12:1 yanasema “Basi ndugu zangu nawasihi kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana.” Sehemu ya maandiko haya ni sehemu inayoonyesha msisitizo juu ya nini ambacho Mungu anafurahishwa kuona tunakifanya katika kuishi kwetu.

Anasema itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, hii umaanisha kuna sadaka zilizo hai na sadaka nyingine ni sadaka zisizo hai mbele za Mungu. Mtume Paulo anazungumza kuwa ili Mungu akukubali ni lazima kutoa mwili wako kuwa dhabihu iliyo hai. Dhabihu iliyo hai katika miili yetu ni kujitoa kwa kila namna na kuruhusu miili yetu itumike mbele za Mungu kwa ajili ya utukufu wake.

Kuitoa miili kuwa dhabihu ni kuruhusu miili yetu kutii na kufuata makusudi ya Mungu, na pia ni kukubali kuishi kwa ajili ya injili. Kama umedhabihu mwili wako mbele za BWANA ni lazima utakuwa radhi kupatwa na jambo lolote kwa ajili ya BWANA na kwenda popote atakapokupeleka na kuacha lolote analokataza na kusema chochote anachokuamuru useme na kutenda lolote atakalo kuambia utende. Wakati mwingine ni kukubali mateso na aibu kwa ajili ya BWANA.

Unapojitoa katika kuifanya kazi ya Mungu kwa moyo na kupenda pasipo kuhimizwa na mtu awaye yeyote hiyo kwa Mungu ni dhabihu iliyo hai, unapofanya kazi ya Mungu kama kuomba, kuhudhuria ibada, kuhubiri/kufundisha, kufanya usafi katika nyumba ya Mungu, kutembelea wagonjwa na wenye shida mbalimbali, kuimba, na kufanya vitu vingi ila kama hautaki kupata sifa za wanadamu bali unafanya kwa ajili ya BWANA hiyo kwa Mungu ni dhabihu iliyo hai.

 Lakini pia anaongezea kusema takatifu ya kumpendeza Mungu. Huku ni kujitoa huku ukiwa na moyo safi mbele za Mungu. Ukitoa dhabihu iliyo hai na katika hali ya usafi wa moyo ni lazima utampendeza Mungu na kujitoa kwako kutakuwa ni ibada yenye maana; watu wengi wamekuwa wakidharau huduma kama kufanya usafi kanisani, kutembelea wenye shida mbalimbali na huduma nyingine ambazo uonekana ndogo ila huku ni kukosa maarifa katika mambo ya Mungu, kwa sababu Mungu anaangalia kama umejitoa kwa kumaanisha huku ukifurahia toka ndani ya moyo wako au unafanya kwa sababu umepangiwa zamu au umelazimishwa na viongozi wako, kama unafanya kwa moyo ni lazima Mungu aihesabu kazi yako kuwa ni kazi iliyo njema na itakuwa ni ibada iliyo njema kwake.

Fanya kila kitu kwa kujitoa kwa moyo na kupenda huku ukifanya ukiwa katika hali ya usafi wa moyo na ukitambua kuwa kila ukifanyacho kwa moyo na kupenda kwa ajili ya BWANA hiyo ni ibada, hata kwa viongozi wa kiserikali wanapofanya mambo katika hali ya usafi wa moyo na kupenda na kufanya kwa ajili ya BWANA, huwa ni ibada yenye maana mbele za Mungu.

Nikukumbushe kuwa kama ni mtakatifu lakini hujatoa mwili wako kuwa dhabihu mbele za BWANA, kwa Mungu hakuna thawabu uipatayo na pia kama unajitoa sana na kufanya mengi sana lakini kama si msafi wa moyo bado unapoteza muda wako na si ibada mbele za Mungu.

Pia ni vyema kufahamu kuwa miili yetu ni hekalu la Roho Mtakatifu na ni vyema kulitunza kwa ajili ya utukufu wa Mungu na kutoruhusu jambo lolote lile litakalo fanya kujinajisi na kuwa mchafu, kwa kuwa Mungu uketi pamoja na walio safi wa mioyo. Ni lazima mwili usiambatanishwe na kitu chochote ambacho ni najisi. Kuwa dhabihu hai mbele za Mungu ni kuuhua mwili katika mambo ya ulimwengu huu na kuuweka wakfu kwa ajili ya BWANA.

Yesu aliwaeleza wanafunzi wake kuwa wakati wa hukumu wapo wengi watakao simama mbele za Mungu na kusema kuwa Bwana sisi tulijitoa sana kwa ajili ya kazi yako lakini Yesu atawajibu na kuwaambia siwajui, ila wapo watakatifu ambao hawakujitoa ambao uzungumzwa kuwa hawataipokea taji ya kazi yao. 

  1. Kutoa muda kwa ajili ya BWANA

Ni ukweli kuwa muda wako ndiyo mafanikio yako, unavyoutumia ndivyo unaonyesha kama utafanikiwa au utashindwa kufanikiwa. Kwenye sura zilizo tangulia tulitazama kuwa matumizi ya muda vibaya ni kikwazo kikubwa cha mafanikio yako. Ila katika sura hii tutatazama kuwa uchoyo wa kumnyima Mungu muda ni kikwazo cha mafanikio ya mtu pia.

ukitazama umuhimu wa mawasiliano kwa wapenzi walio ndani ya ndoa na hata wanaokaribia kuoana, utagundua kuwa mazungumzo imara ya mara kwa mara ndio ubora wa mahusiano na hata ndoa kwao. Na ukimpatia mpenzi wako muda mdogo au ukimnyima kabisa muda wa kuzungumza nawe ni lazima utakuwa unaelekea kwenye hatari ya kuvuruga mahusiano yako au ndoa.

Jambo hili linauhusiano sana na Mungu wetu kuwa anapenda tuwe na muda naye na kuzungumza naye na hata kufurahi naye, ila tunapomnyima muda wa kukaa nasi ni kujitengenezea maangamizo yetu wenyewe na wakati mwingine ni kuvunja ukaribu kabisa naye. Kama uwezavyo kumtengea mpenzi wako au rafiki zako muda wa kuzungumza nao ndivyo unapaswa kumtolea Mungu sadaka ya muda wako. Fahamu ya kuwa muda unaoutoa mbele za Mungu ni sawa na sadaka na kama ukitoa vyema na kwa moyo wa kupenda ni lazima Mungu akubariki.

Waefeso 5:15-16 “Basi angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima; 16 mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu.” Tuna wakati mdogo sana ila ni lazima tuwe makini tunavyoutumia, epuka kutumia muda wako kama wasiomjua Mungu wanavyoutumia, kwa kuwa wao hawana hata muda wa kukaa na Mungu hata kidogo, ila kama watu wenye hekima za Mungu ni vyema kuukomboa wakati(kufanya mambo ya maana tu ambayo ni mema hata mbele za Mungu)

Visingizio ni ishara ya kupotea, epuka kila wakati kutoa visingizio kwa kuwa hivyo vilikuwepo, vipo na vitaendelea kuwepo ila waweza kuvishinda kwa kujikana wewe mwenyewe. Kuna watu ushindwa kumfanyia Mungu ibada kwa kuwa na visingizio kuwa hawana muda, muda huwa haukamatiki mkononi, na kama ukisubiri kuupata muda kamwe hautoweza kuupata, ila ukiamua kuutumia uliopo ni lazima utafaulu kufanya hata yasiyowezekana.

Acha visingizio kuwa una mambo mengi kwa kuwa hayatakuja kutokea yakawa machache ili upate muda wa kukaa na Mungu wako, pia ukisema una ratiba ngumu inayokunyima muda na Mungu ujue kuwa haitakuja tokea hiyo ratiba ikawa rahisi mpaka umeirahisisha kwa kuchukua maamuzi magumu ya kuwa na muda na Mungu.

Jiulize kuwa mbona mambo mengine unafanya lakini kwenye suala la Mungu tu ndipo unakosa muda, hii ni ishara ya kuwa Mungu kwako si muhimu kama vilivyo vitu vingine. Ni vyema kuweka msimamo wako wa kuwa na muda wako na Mungu na epuka kutokea kitu kingine kukuvurugia. Kama ilivyo kwa mtu wa karibu yako hauoni raha akiwa mbali au usipo wasiliana naye, ndivyo wapaswa kujisikia kwa Mungu kama haujawasiliana naye au kumtafuta na uhuzunike na kuugua sana.

Kama mtu mwenye shauku ya kumjua Mungu na kufanikiwa katika mambo yote ni lazima utumie vyema muda wako, kwa kuwa na ratiba ya kuhudhuria ibada zilizopo, na kuwa na ibada yako binafsi ambapo utamsifu, kumuabudu, kujifunza neno na kuomba Mungu.

Mathayo 26:40-41 “Akawajia wale wanafunzi, akawakuta wamelala, akamwambia Petro, Je! Hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja. 41 Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho I radhi lakini mwili ni dhaifu”

Yesu anawaambia wanafunzi wake wangekesha hata saa moja, ni vyema kufanya jambo hili kudumu na BWANA hata saa moja kama mambo ni mengi kwa kuhudhuria ibada na wakati mwingine saa laweza likawa jingi ila Mungu anajali sana muda ulioweka kuwasiliana naye.

Muda ni sadaka ambayo unapaswa umtolee Mungu na epuka kutumia muda wote ndani ya siku pasipo kumpa BWANA muda wake.

  1. Kumtolea Mungu fedha na mali. 

Eneo jingine lililo la muhimu sana katika maisha ya mwamini ni eneo la utoaji wa fedha na mali kwa ajili ya Bwana. Eneo hili ni muhimu sana kwa kuwa ni sababu kubwa sana ya Mungu kubariki watu wake na kwa mtu ambaye amekosa uaminifu katika hili eneo ukaaa chini ya laana ila kwa aliye mwaminifu uwa ndani ya Baraka.

Kuna aina mbali mbali za utoaji wa fedha na mali, aina hizo ni kama:

  1. Sadaka ya kuwasaidia watu walio katika uhitaji.

Hii ni sadaka ya mtu kumsaidia mtu haswa Yule ambaye hana matumaini na hana msaada kwa kutoa vile alivyonavyo na kumpatia. Hii ni sadaka ya upendo kwa kuonyesha kumpenda Mungu na kumpenda Yule unayemsaidia.

Hii ni sadaka ambayo mtu anaifanya mbele za mtu kwa ajili ya Mungu, na ikifanyika kwa mtu kujitakia utukufu wake huwa haina thawabu mbele za Mungu ila ikifanyika kwa moyo wa kupenda na kumtukuza Mungu ni njema na ubeba thawabu kubwa mbele za Mungu.

Luka 6:38 “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa kifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakacho pimiwa.”  Yesu anapotoa neno hili anazungumza na watu walioamini kuwa imewapasa kutoa vitu vyao kwa watu(wenye uhitaji) ila kutoa kwao si bure kwa kuwa ni lazima Mungu atawarudishia tena  kupitia watu,  si kama walivyotoa bali ni zaidi kwa kipimo cha kujaa  na kushindiliwa na kusukwa-sukwa hata kumwagika.

Mfano wa sadaka hii katika biblia ni:

  • Sadaka ya Rahabu kujitoa na kujihatarisha ili wapelelezi kutoka Israeli wapone.

Kitabu cha Yoshua 2:1-6

  • Sadaka ya BWANA Yesu kwetu wanadamu.

Kitabu cha Isaya 53

  • Sadaka ya mjane wa Sarepta kwa Eliya.

Kitabu cha 1 Wafalme 17:13-16 “

  • Sadaka ya Kornelio kwa watu wenye shida mbali.

Kornelio alikuwa mtoaji sana na aliwapa watu sadaka nyingi sana, kama inenavyo katika Matendo ya mitume 10:2 “mtu mtauwa, mchaji wa Mungu, yeye na nyumba yake yote, naye alikuwa akiwapa watu sadaka nyingi, na kumwomba Mungu daima.

Sadaka ya mtu kujitoa na kutoa vitu vyake vya thamani ni sadaka yenye thamani sana mbele za Mungu na ni ishara ya kuwa mtu anampenda Mungu na yule anayemsaidia.

  1. Sadaka kwa ajili ya kuendeleza kazi ya Mungu.

Sadaka hii huitwa kwa majina mengi, na wengine huiita sadaka ya lazima. Wengine matoleo, wengine upenda kuiita sadaka ya ibada. Hii sadaka utolewa kila watu wa Mungu wakutanikapo pamoja kufanya ibada, na mlengo mkuu wa sadaka hii ni kuiendeleza kazi ya injili ipate kusonga mbele.

Ni sadaka ambayo utumika kuimalisha miundombinu ya kanisa, na pia kuwa saidia watumishi wa Mungu, na shughuli nyingine nyingi kama ilivyopangwa na kanisa husika la mahali pamoja. Hii ni sadaka muhimu sana na ni ya lazima kwa kila muumini kuangalia kuitoa kila anapokuwepo ibadani.

Hii ndiyo sadaka inenewayo kuwa usiingie nyumbani kwa BWANA mikono mitupu.

  1. Sadaka ya malimbuko.

Hii ni sadaka ambayo ni ya mwanzo wa kila pato ulipatalo katika yale uyafanyayo. Kama ni biashara basi yale mapato ya kwanza ni malimbuko yako kwa BWANA, kama ni kazi huwa mshahara wa kwanza, kama ni mazao uwa yale ya kwanza na vivyo hivyo kwa wanyama. Sadaka hii pia kwa nyakati za leo uwasilishwa kanisani.

  1. Sadaka ya shukrani

Kitabu cha Zaburi 50:14

Hii ufanywa kwa lengo la kumshukuru Mungu kwa lile lililotokea katika maisha liwe zuri au baya.

Mwalimu Mwakasege anaielezea kuwa ni sadaka ya muhimu kuifanya kila wakati unapofanyiwa jambo au unapokumbwa na jambo, na uelezea kuwa hii ni sadaka ya msingi sana kumshawishi Mungu azidishe utendaji wake katika maisha ya mwamini.

 Zaburi 50:5

Matendo ya Mitume 5:1-11

  1. Fungu la kumi.

Malaki 3:8-12

Hii ni sehemu ya kumi ya mapato yako yote uyapatayo, ni  sadaka muhimu sana ambayo pia ipo kwa ajili ya kuiendeleza kazi yake.

–Na Mwl Kelvin Kitaso

No comments: